
Kushoto ni mchezaji Job Ibrahim na kulia ni Ayoub Siwelo Mwenyekiti wa kamati ya usajili Lipuli FC.
Usajili wa Job Ibrahim ambaye aliwahi kuchezea klabu ya Yanga, umeifanya Lipuli kufikisha jumla ya wachezaji watano mpaka sasa huku dirisha la usajili likitarajiwa kufungwa rasmi Julai 27.
Akiongea na www.eatv.tv , Afisa habari wa klabu hiyo, Clement Sanga amesema.
“Hizo ni taarifa za kweli na ni katika harakati za kuboresha kikosi chetu ikizingatiwa kwamba msimu ujao wa ligi utakuwa na mechi 38 kwahiyo kazi inaendelea , hivi sasa bado nafasi za magolikipa wawili ambao tunawahitaji ili tuwe vizuri zaidi“.
Wachezaji wengine waliosajiliwa na klabu hiyo ni William Lucian ‘Gallas’ kutoka Ndanda Fc, Miraj Madenge na Paul Nonga wa Mwadui Fc wote wakisaini kataba wa mwaka mmoja, pamoja na Issa Ally Rashid ambaye amesaini mkataba huru wa miaka miwili.
Pia Sanga amethibitisha kuwa kocha Selemani Matola amesaini mkataba wa mwaka mmoja wiki iliyopita kuitumikia klabu hiyo kama kocha msaidizi huku wakisubiri kumsaini kocha mkuu muda wowote kuanzia sasa.
Lipuli Fc ilifanikiwa kusalia katika ligi kuu msimu uliopita ambao ni msimu wake wa kwanza huku klabu ya Mji Njombe na Majimaji za ukanda huo wa nyanda za juu Kusini zikiteremka daraja.