Uwanja wa Kambarage Shinyanga Stand United itamkaribisha Simba SC huku Mkwakwani mkoani Tanga Mgambo akishuka dhidi ya African Sports ambapo Uwanja wa Sokoine Mbeya City itashuka dhidi Toto Africans kwa upande wa Ndanda atamkaribisha Majimaji Uwanja wa Nangwanda sijaona mjini Mtwara na Karume jijini Dar es salaam JKT Ruvu itamkaribisha Kagera Sugar.
Akizungumza na East Africa Radio mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura amesema, kwa kawaida kunakuwa na mechi nane katika mzunguko mmoja lakini mechi moja imepungua kutokana na Yanga walioondoka leo hii kuelekea nchini Mauritius kushiriki mechi Klabu bingwa Afrika.
Mzunguko huo utahitimishwa siku ya Jumapili kwa michezo miwili ambapo Coastal Union itaikaribisha Azam FC Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na Mwadui FC itawakaribisha wajelajela Tanzania Prisons Uwanja wa Mwadui mjini Shinyanga.
Kwa upande mwingine Wambura amesema, kuhusu suala la kadi nyekundu ya beki wa kati wa klabu ya Yanga Kelvin Yondani wameangalia ripoti ya mwamuzi na kamishna wa mchezo waliochezesha mchezo dhidi ya Coastal Union jijini Tanga na imethibitisha kuwa Yondani alimpiga Daktari wa Coastal Union kwa kutumia boksi la huduma ya kwanza.
Wambura amesema, kwa mujibu wa kanuni ya udhibiti wa wachezaji ya ligi kuu Yondani anaendelea kuitumikia kadi yake nyekundu ambapo mechi ya mwisho ataimalizia kwa kutocheza mchezo dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC pamoja na kulipa faini ya shilingi laki tano.
Wambura amesema, kamati ilikwenda mbele zaidi kwa kuangalia ripoti ya kamishna na mwamuzi ambayo ilionesha kuwa daktari wa Coastal Union Mganga Kitambi alimpiga ngumi Yondani ambapo suala lake limeangukia moja kwa moja kwenye masuala ya utovu wa nidhamu hivyo linapelekwa kwenye kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka nchini kwa ajili ya hatua zaidi.




