Jumanne , 30th Oct , 2018

                                 
Uongozi wa klabu ya Leicester City umesema kuwa uko katika majadiliano juu ya kubadili jina la uwanja wake kutoka 'King Power' inalotumia sasa na kuwa katika jina la mmiliki wa klabu hiyo, Vichai Srivaddhanaprabha aliyefariki kwa ajali ya helikopta.

Uwanja wa Leicester City, King Power

Mmiliki huyo wa Leicester City na wengine wanne wameripotiwa kufariki katika ajali ya ndege nje ya uwanja wa klabu hiyo, ajali iliyotokea Jumamosi ya Oktoba 27 baada ya kumalizika kwa mchezo wa EPL kati ya Leicester City na West Ham United, mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 .

Mtoto wa tajiri huyo aitwaye, Aiyawatt ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Leicester City ndiye atakayechukua nafasi yake kwa muda, ambapo anatarajia kukutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa klabu, Susan Whelan kuhusiana na namna nzuri ya kumuenzi mmiliki huyo wa klabu.

"Uwanja wa King Power ni matokeo ya mafanikio kutokana na uwekezaji wa Khun Vichai, tutafungua rasmi majadiliano na familia, klabu na mashabiki kwaajili ya jina la uwanja wetu, litakalomuenzi Khun Vichai", imesema taarifa ya klabu hiyo.