
Shirikisho la masumbwi ya kulipwa Tanzania PST, limeruhusiwa na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kuendelea na shughuli zake, baada ya kusimamishwa na Baraza la michezo Tanzania BMT, kwa kuchezesha watoto chini ya umri wa miaka 10 kwenye mapambano yake.
Katibu Mkuu wa PST, Anthony Ruta, amesema wataendelea na shuguli zao, hadi hukumu itakapotoka, lakini pia wanajiandaa kwenda kwa Waziri wa habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye, kumshitaki katibu Mkuu wa BMT, Mohammed Kiganja kwa madai ya kutumia vibaya madaraka yake.
BMT iliifungia PST, kwa kuchezesha watoto wenye umri chini ya miaka 10 na kumuajiri mnadi miunguko(Card Girl) mtoto mwenye umri chini ya miaka nane kinyume na sheria.
Mbali na kufungiwa kwa shirikisho hilo pia Serikali ilisitisha uteuzi wa Emmanuel Mlundwa kama mjumbe wa kamati ya kutengeneza katiba, kanuni na taratibu za kufuatwa katika michezo ya ngumi za kulipwa.
Akitoa tamko hilo Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Mohammed Kiganja alisema kuwa Katika pambano lililofanyika Mei 14 kati ya Thomas Mashali na bondia wa Iran, Sadjadi Meherab, PST iliwachezesha watoto hao huku kitendo kama hicho pia kikiwahi kutokea Juni 18 mwaka 2002. "Katika pambano hilo PST walimtumia mtoto Joyce Francis ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi kama mnadi mizunguko katika pambano hilo", alisema Kiganja.