Jumatano , 24th Oct , 2018

Kocha mkuu wa klabu ya Simba Mbelgiji, Patrick Aussems, amesema mwendelezo wa kiwango kizuri cha Aishi Manula tangu msimu huu uanze ndio sababu kubwa ya mlinda mlango namba mbili wa Simba Deogratius Munishi maarufu Dida kukaa benchi.

Deogratius Munishi (kushoto) na Aishi Manula (kulia).

Akiongea kuelekea mchezo wa timu yake leo dhidi ya Alliance FC Aussems ameweka wazi kuwa ana walinda lango wengi kwenye kikosi chake akiwemo Dida lakini hawawezi kucheza wote na Manula yupo kwenye kiwango bora ni vyema akaendelea kucheza.

''Simba inakabiliwa na michuano mingi msimu huu ikiwemo ya kimataifa, hivyo uhakika wa kumtumia Dida na walinda mlango wengine kikosini ni mkubwa lakini watatumika kutokana na mazingira yatakavyoruhusu'', ameeleza.

Dida alirejea nchini mwezi Julai mwaka huu akitokea Afrika kusini na kujiunga na mabingwa hao. Tangu kuanza kwa msimu huu bado hajapata nafasi ya kucheza katika michezo ya ligi kuu.

Simba ambayo inashika nafasi ya 3 ikiwa na alama 17 leo inashuka dimbani kukipiga na Alliance FC kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam. Alliance inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo ikiwa na alama 6 baada ya kucheza mechi 10.