Jumanne , 25th Oct , 2016

Aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi cha Yanga SC Hans Van Der Pluijm leo amewaaga rasmi wachezaji wa timu, ikiwa ni siku moja baada ya kujiuzulu kukinoa kikosi hicho.

Kocha Hans akiagana na wachezaji wa Yanga

Hans alifika kwenye mazoezi na kuongea na wachezaji wote pamoja na benchi zima la ufundi kisha akawaacha wakiendelea na mazoezi yao.

Klabu ya Yanga SC ilikubaliana na ombi la kocha huyo kujiuzulu huku ikikanusha habari zilizoenea kuwa kocha msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa Makipa Juma Pondamali na Meneja Hafeedh Saleh watajiuzulu nafasi zao ndani ya klabu hiyo.

Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deusdedit amesema, kamati ya utendaji na uongozi wa Yanga kwa ujumla wanapitia majina ya makocha takribani sita yaliyofika mezani kwao huku akiwataka mashabiki kuwa na utulivu kwani hicho ni kipindi cha mpito na anaamini uongozi utatafuta mtu sahihi wa kuchukua nafasi ya Hans Van der Pluijm.

Pluijm amejiuzulu siku chache mara baada ya kuenea kwa habari kwamba klabu hiyo imeleta kocha mpya, Mzambia George Lwandamina.

George Lwandamina - Anayetajwa kurithi mikoba ya Hans

 

Hiki kilikuwa ni kipindi cha pili kwa pluijm kuifundisha Yanga baada ya awali kufundisha kwa nusu msimu mwaka 2014, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts.

Baadaye alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa katika mwezi wa Januari mwaka jana. 

Marcio Maximo - Aliyekuwa Kocha wa Yanga kabla ya kurejea kwa pluijm

 

Nchini Saudi Arabia ambako alikwenda na aliyekuwa Msaidizi wake, Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa – Pluijm  aliondoka baada ya kutofautiana na uongozi wa timu uliotaka kumsajilia wachezaji asiowataka.

Franciscus Johannes ‘Hans’ van der Pluijm alizaliwa Januari 3 mwaka 1949 na alianzia kwenye kucheza soka akiwa kipa.

Enzi zake aliidakia kwa miaka 28 klabu ya FC Den Bosch akicheza mechi 338 ndani ya misimu 18 na alipostaafu baada ya kuumia goti akawa kocha wa timu hiyo.

Alianza vyema ukocha akiiwezesha FC Den Bosch kutwaa ubingwa wa Daraja la Kwanza na kupanda Ligi Kuu na ndiye aliyempa nafasi ya kwanza mshambuliaji Ruud van Nistelrooy akiwa kinda wa miaka 17 tu kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Ruud van Nistelrooy

 

April mwaka 1995, alisaini Mkataba wa miaka miwili na SBV Excelsior kabla ya kutimuliwa Januari 1997 na nafasi yake ikachukuliwa na Msaidizi wake, John Metgod. 

Hiyo ilifuatia timu hiyo ya Rotterdam kushinda mechi mbili tu na sare tatu katika mechi 17 za msimu mzima.
Baada ya kuboronga Ulaya, ndipo akahamia Afrika mwaka 1999, alipokwenda kufundisha Ashanti Gold SC ya Ghana, akianza na Mkataba wa mwaka mmoja. 

Ashanti Gold SC

Ajax ya Uholanzi ikanunua hisa katika klabu hiyo Ijumaa ya Juni 18, mwaka 1999 asilimia 51 naye akatupiwa virago na kuhamia Saint-George SA ya Ethiopia kabla ya mwaka 2010 kujiunga na B-Juniors Feyenoord ya Ghana, ambayo ni tawi la timu hiyo ya Rotterdam.

Mwaka 2012 alijiunga na Berekum Chelsea ambako pia alifukuzwa mwaka juzi na kuhamia Medeama ya Ghana pia ambako nako alifukuzwa baada ya mechi saba tu, kufuatia matokeo mabaya mwanzo mwa msimu, akivuna pointi nane kati ya 21.

Pluijm anaondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 124, akishinda 77, sare 25 na kufungwa 22.

Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 106 za tangu mwaka jana, alishinda 67, sare 19 na kufungwa 20.