Jumatatu , 14th Nov , 2016

Shirikisho la Soka Afrika Kusini (SAFA), limemsimamisha Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya nchini hiyo, maarufu kama Bafana Bafana, Ephraim ‘Shakes’ Mashaba, masaa 24 tu baada ya kuiongoza timu hiyo kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Senegal.

Rais wa SAFA Danny Jordaan (kushoto) akishikana mikono na Ephraim Mashaba kipindi anapewa kazi

 

SAFA imetoa maelezo ya kumsimamisha Mashaba kwa madai ya kumtusi Rais wa SAFA, Danny Jordaan‚ kwa kuonesha alama ya vidole, baada ya ushindi huo wa 2-1 dhidi ya Senegal, katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia, mwaka 2018 nchini Urusi uliopigwa Polokwane Jumamosi iliyopita.

SAFA, imesema suala lake lipo kwenye Kamati ya Maadili, na kwa sasa timu ya Bafana Bafana, itakuwa chini ya Kocha Msaidizi Owen da Gama‚ ambaye ataisimamia timu hiyo kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Msumbiji kesho katika uwanja wa Estadio do Zimpeto mjini Maputo.

Mashaba amekuwa akinukuliwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari kuwa Rais wa SAFA, Jordaan hampi ushirikiano kama kocha wa Bafana Bafana.