Ijumaa , 21st Sep , 2018

Klabu ya manispaa ya Kinondoni (KMC) imepata ushindi wake wa kwanza wa ligi kuu Tanzania bara hii leo dhidi ya Stand United, mchezo ambao umepigwa katika uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Kikosi cha KMC, wenye jezi Nyeupe kikishambulia dhidi ya Stand United wenye jezi za rangi 'orange'.

Mchezo huo ambao ni wa tano kwa KMC, umemalizika kwa klabu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya ‘Wapigadebe’ hao, mabao yaliyofungwa na, Massoud Abdallah katika dakika ya 10 na Emmanuel Mvuyekure katika dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza ya mchezo huo.

Ushindi huo ni wa kwanza kwa KMC katika ligi kuu msimu huu baada ya kushuka dimbani mara tano, ikitoa sare mechi tatu na kufungwa mchezo mmoja na Singida United wikiendi iliyopita.

Kwa matokeo hayo, inafikisha alama sita na kukamata nafasi ya 11 ya msimamo wa ligi sambamba na Kagera Sugar na Lipuli Fc zenye alama hizo katika michezo yake minne iliyoshuka dimbani mpaka sasa.

Stand United imepoteza mchezo wa pili mfululizo baada ya kufungwa katika mchezo wa wikiendi iliyopita kwa mabao 4-3 na mabingwa wa kihistoria Yanga katika uwanja wa taifa.