Jumamosi , 6th Feb , 2016

Kiungo Wekundu wa Msimbazi Simba Said Juma Ndemla amewaondoa shaka mashabiki wa timu hiyo juu ya kiwango na uwezo wake kiuchezaji mara baada yakuonekana akianzia benchi katika michezo kadhaa sasa ya klabu hiyo.

Ndemla kwa sasa hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Simba na mara nyingi amekuwa akiingia akitokea benchi huku Kocha Jackson Mayanja akiwatumia zaidi viungo Jonas Mkude na Mzimbabwe Justice Majabvi.

Kutokana na hali hiyo, Ndemla amesema hatishwi na kuwekwa benchi kila mara kwani anajijua anamudu kucheza nafasi tano uwanjani na ameamua kujifua zaidi ili arudi first eleven.

Ndemla amesema anamudu kucheza kiungo namba sita, kiungo mashambuliaji namba nane, winga ya kulia na kushoto, hata mshambuliaji msaidizi, yaani namba 10 hivyo kujifua kwake ni katika hali ya kumshawishi mwalimu kumpaka katika moja ya nafasi hizo.

Ndemla amekuwa akijiuliza maswali mengi mfano nanukuu “Sijui kwa nini kocha hanitumii, ila yeye ndiye anayejua mahitaji ya kikosi, mimi sihitaji kumuingilia katika hilo. Ila kwa upande wangu, kwa kuwa nacheza nafasi tano za viungo uwanjani, nitahakikisha narejea kikosini, kwanini nipate namba taifa stars nishindwe Simba?.

Ndemla akaenda mbali zaidi nakusema kuwa “Nitaongeza bidii katika mazoezi ili niweze kumshawishi kocha anipe nafasi ya kuanza kikosini, ninachotaka ni kurudi kikosini, sitajali kuhusu nafasi gani atanipanga kwakuwa najua namudu nafasi tano kiwanjani,”.

Kuhusiana na hilo, Mayanja alisema: “Ndemla ni mchezaji mzuri lakini bado naendelea kumuandaa, haiwezekani wakacheza wachezaji wote, kumbuka kuna mifumo na falsafa katika soka, hivyo Ndemla ananafasi yake kama wengine na isitoshe kwa mfumo wangu wa sasa Ndemla anafaa zaidi kuingia akitokea benchi ili kubadili mchezo na kumaliza kabisa wapinzani.

Ndemla ambaye kwa sasa yuko na timu hiyo kanda ya ziwa kwa michezo miwili ya ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar hapo kesho katika Dimba la Kambarage na baadae dhidi ya Stand United katika uwanja huo huo ni mmoja wa viungo bora chipukizi ambao ni zao la timu ya Simba akitokea katika kikosi cha pili cha timu hiyo.