
Kocha mpya wa Ihefu, Zuberi Katwila akizungumza na Waandishi wa Habari.
Katwila, amejiunga na Ihefu ikiwa ni saa chache tangu kujiuzulu kwake kuifundisha Mtibwa Sugar ambayo alidumu nayo kwa miaka mitatu akiwa na wakatamiwa hao ambao aliwasaidi kutwaa mataji mawili yasiyo ya ligi kuu.
Mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa na Taifa Stars, aliondoka jana kufuatia mfululizo wa matokeo yasiyo mazuri ambapo katika mechi sita, kashinda moja, sare moja na vipigo vitatu mfululizo.
Amejiunga na Ihefu ambayo nayo katika mechi sita, imeshinda moja pekee na kufungwa michezo mitano, kiasi cha kuamua kumfuta kazi Maka Mwalwisi ambaye aliisaidia timu hiyo kupanda ligi kuu wakitokea daraja la kwanza.
Changamoto kubwa ambayo atakumbana nayo Zuberi ni kuhakikisha anarejesha hali ya ushindi kikosini, kwakuwa imani kubwa ya wamiliki wa Ihefu ni kwamba Katwila anauzoefu wa kutosha wa ligi, na anajua namna ya kupata alama.
Inawezekana akiwa na Mtibwa Sugar, filosofi ya kutegemea vijana wanaopandishwa katika mashamba ya miwa, ilimnyima nafasi Katwila kutengeneza timu ya ushindi, lakini Ihefu inatajwa kuwa ni timu yenye wawekezaji ambao wanakiu na mafanikio hivyo huenda wakatenga bajeti kwa ajili ya usajili ya wachezaji watakaofanikisha malengo hayo.
Cha kuzingatia kwa sasa Zuberi atacheza michezo ya VPL iliyosalia kabla ya dirisha dogo la usajili kwa kutegemea wachezaji waliopo, na wengi wanatarajia kupitia ubora wake unaweza ukabadili hali ya kushindwa uliopo kwa sasa ndani ya kikosi cha Ihefu na ndicho kipimo chake cha kwanza.
Jambo la msingi kwa viongozi wa Ihefu ni kumpa muda Zuberi Katwila na kutotegemea matokeo ya haraka ndani ya muda mfupi, pia wamtengenezee mazingira ya kufanya kazi kwa uhuru na ushirikiano ili wapate wanachokusudia.
Ihefu haikufanya maingizo mapya mengi katika kikosi kilichowasaidia kupanda ligi kuu, jambo ambalo linaweza kuwa sababu ya kushindwa kuhimili vishindo vya VPL, hivyo watumie dirisha dogo la usajili kumuongezea Katwila wachezaji wenye uzoefu ambao watasaidia kupambana katika mechi zijao.