Jumatatu , 7th Jul , 2014

Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa ya vijana ya Tanzania wenye umri chini ya miaka 17 Serengeti Boyz Hababuu Ally amepongeza mazingira mazuri ya kambi ya timu hiyo, maandalizi na ushirikiano mkubwa wanaopata toka shirikisho la soka nchini TFF

Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa ya vijana ya Tanzania walio na umri chini ya miaka 17 Serengeti Boyz mzalendo Hababuu Ally amesema utulivu na huduma nzuri katika kambi ya timu hiyo iliyo katika hostel za shirikisho la soka hapa nchini TFF maeneo ya karume jijini Dar es salaam inampa matumaini ya kikosi chake kuibuka na ushindi dhidi ya vijana wa Afrika kusini katika mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza michuano ya Afrika ya umri huo itakayofanyika mwakani nchini Niger

Aidha Hababuu amesema hivi sasa amebakiza wachezaji 28 katika kikosi cha timu hiyo baada ya kuwachuja wengine kutoka katika idadi ya wachezaji 40 wa awali na waliobaki wanataraji kucheza michezo miwili ya kirafiki ili kupima uwezo wa kikosi hicho

Ambapo kocha huyo amesema kesho asubuhi timu hiyo inataraji kucheza mchezo wa kirafiki na timu iliyopanda daraja msimu huu ya maafande wa Polisi Morogoro mchezo ambao utapigwa katika uwanja wa kumbukumbu ya karume jijini Dar es salaam na baadae mwishoni mwa juma timu hiyo itavaana na timu ya vijana wa umri wa chini ya miaka 20 ya Azam FC katika uwanja wa Azam complex Chamazi ulioko nje kidogo ya jiji la Dar es salaaam mechi zote zikiwa na lengo la kuangalia mapungufu ya timu hiyo na kuyarekebisha kabla ya kuvaana na vijana wenzao wa Afrika kusini.

Na Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo Athanas Mdam amesema wao kama wachezaji wako katika Morali ya hali ya juu kwakuwa kila mmoja anafahamu umuhimu wa mchezo huo dhidi ya Afrika Kusini na pia wachezaji wote wana hamu kubwa ya kwenda kwenye michuano hiyo huko Niger hapo mwakani