Jumamosi , 17th Feb , 2018

Baada ya kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu nyota wa kimataifa wa klabu ya Singida United, Papy Kambale hatimaye leo amerejea kikosini na kuichezea timu hiyo kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar.

Pamoja na kurejea leo Kambale ameibuka shujaa wa Singida United, baada ya kusawazisha bao na kuiwezesha timu hiyo kuondoka na alama moja kwenye mchezo uliomalizika jioni hii kwenye uwanja wa Kaitaba Bukoba.

Katika mchezo huo wa ligi kuu raundi ya 19, Kagera Sugar ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 33 kupitia kwa nyota wake Mohamed Fakhi kabla ya Kambale kusawazisha dakika ya 49.

Nyota huyo raia wa DR Congo alisimamishwa na klabu yake mapema mwezi uliopita baada ya kufanya kosa la kumpiga mchezaji wa Green Worriors kwenye mchezo wa Kombe la shirikisho.

Baada ya sare ya leo Singida United imeendelea kusalia katika nafasi ya nne ikiwa na alama 34 nyuma ya Azam FC yenye alama 35 nafasi ya tatu, Yanga yenye alama 37 nafasi ya pili na Simba yenye alama 42 kileleni.