Jumamosi , 9th Jun , 2018

Kuelekea Fainali za 21 za Kombe la Dunia nchini Urusi, ni mataifa 7 ambayo yanashiriki kati ya 32 yakiwa tayari yameshawahi kutwaa ubingwa wa Dunia yakisaka kuongeza idadi ya taji hilo katika kabati zao.

Taifa ambalo linaongoza kwa kuchukua mara nyingi, Brazil wao watakuwa wanatafuta ubingwa wao wa sita baada ya kutwaa mara tano katika miaka ya 1958, 1962, 1970, 1994 na 2002. Mwaka huu wakiwa na nyota wao vijana kama Neymar wanapewa nafasi ya kutwaa ubingwa.

Anayefuatia kwa kuchukua ubingwa huo mara nyingi ni nchi ya Ujerumani, ambao wamechukua mara 4 huku wakiwa ndio mabingwa watetezi baada ya kutwaa mwaka 2014 nchini Brazil bado wakiwa na kizazi chao cha dhahabu kama Muller na Ozil wanapewa nafasi ya kutetea.

Timu zinazofuatia ni Uruguay ambao ni mabingwa wa kwanza wa Kombe la Dunia mwaka 1930 pamoja na Argentina zikiwa zimetwa mara mbili kila mmoja. Nchi hizo zina nyota kama Suarez kwa Uruguay na Messi kwa Argentina na zinapewa nafasi ya kuongeza taji.

Kwenye orodha ya waliowahi kuchukua ubingwa kati ya timu 32 za mwaka huu, Uingereza na Ufaransa wanafunga wakiwa wametwaa taji moja moja. Mwaka huu wa vikosi vyenye vijana wengi wanaofanya vizuri ngazi ya klabu na zinatajwa kuwa miongoni mwa timu zenye nafasi ya kuchukua ubingwa.