Jumamosi , 9th Jun , 2018

Baada ya kuwa kimya kwa muda akiendelea na matibahu ya bega aliloteguka kwenye mchezo wa fainali ya UEFA, mchezaji wa Liverpool na Misri Mohamed Salah amesema kwa jinsi anavyoendelea yupo tayari kucheza mechi ya ufunguzi dhidi ya Uruguay.

Kauli ya Mo Salah imeipa nguvu nchi ya Misri baada ya kumhakikishia Rais  Abdel Fattah el-Sisi,  kuwa yuko tayari kuichezea nchi hiyo kuanzia mechi yake ya kwanza kwenye Fainali zinazoaanza Juni 14 nchini Urusi.

''Ninajisikia vizuri kwasasa, nahisi nipo tayari kucheza mechi yetu ya ufunguzi kwenye Kombe la Dunia dhidi ya Uruguay na ninaamini nitacheza vizuri na kuisaidia timu yangu'', Mo Salah amemwambia Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi.

Misri ambayo ipo kundi A na wenyeji Urusi pamoja na nchi za Uruguay na Saudi Arabia, itaanza kampeni zake za kusaka ubingwa dhidi ya Uruguay Juni 14, kabla ya kucheza na wenyeji Juni 19 na kumaliza mechi zake za makundi dhidi ya Saudi Arabia.

Salah ambaye msimu wa 2017/18  ameibuka mfungaji bora wa ligi kuu ya England kwa kufunga mabao 31, aliteguka bega kwenye mchezo wa Fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Real Madrid kufuatia kukumbana na mlinzi Sergio Ramos.