Jumanne , 13th Jul , 2021

Uongozi wa klabu ya Yanga umewataka mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo wake dhidi ya Ihefu wa VPL utakauochezwa Julai 15 kwenye dimba la Mkapa ili kumuaga kiungo wake wa kimatifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima ambaye anamaliza mkataba wake msimu huu.

Haruna Niyonzima akijaribu kumtoka mlinzi wa Polisi Tanzania, Detus Peter wakati wawili hao walipokutana kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa VPL ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1 kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Yanga wameandika hayo kupitita ukurasa wake wa Instagram na kuipa heshima siku hiyo mahususi kwa kuiita 'Niyonzima Day'.

Ikumbukwe kuwa Haruna Niyonzima alijiunga na Yanga mwaka 2011 akitokea klabu ya APR ya nchini Rwanda na kucheza kwa mafanikio makubwa hadi Julai mwaka 2017 ambapo alitimkia kwa watani wake wa jadi, Simba.

Niyonzima alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga kwa kuonesha uhodari wake wa kupiga pasi mpenyezo na madoido mengi akitokea eneo la kiungo mchezeshaji na hatimaye kuisaidia Yanga kubeba mataji yasiyopungua matatu ya Ligi kuu, moja la Shirikisho na kushiriki michuano ya Afrika.

Nyota huyo alianza misuguano ya kinidhamu na klabu yake ya Yanga hususani kuchelewa kurejea klabuni pindi aendapo nchini kwao Rwanda na baadae kutimkia Simba ambapo alifanikiwa kutwaa mataji mawili ya VPL na kuisaidia Simba kufika robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika.

Baada ya mkataba wake kumalizika kwa wekundu wa msimbazi Simba, Niyonzima akarejea Yanga mwezi Januari 2020 ambapo ameitumikia timu hiyo ya kwa mwaka mmoja na nusu, jumla ya miaka takribani saba ya mafanikio akiwa timu ya Wananchi.