Jumanne , 25th Nov , 2025

Nyota wa Klabu ya Everton Idrissa Gueye ameomba radhi kwa Nohodha wake Michael Keane mara baada ya hapo jana kumpiga kibao katika mchezo wa EPL walioibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Man United katika Uwanja wa Old Trafford.

Mwamuzi akimuonyesha Gueye kadi nyekundu

Idriss alimpiga kibao ndani ya dakika 15 tu za mchezo kipindi cha kwanza baada ya kupishana kauli kwenye majukumu ya kiulinzi wakati Everton ilipokuwa inashambuliwa. Tukio hilo lisilo la kiungwana lilimfanya Mwamuzi wa mchezo huo, Tony Harrington kumtoa nje Nyota huyo raia wa Senegal katika dakika ya 13 na kucheza pungufu kwa dakika 77 Uwanjani.

Kupitia mtandao wake wa Instagram pamoja na X (Twitter), Idriss amesema  "Naomba msamaha kwanza kwa mchezaji mwenzangu Michael Keane. Pia ninaomba msamaha kwa wachezaji wenzangu, wafanyakazi, mashabiki na klabu,"

"Kilichotokea hakiakisi mimi ni nani au maadili ninayosimamia. Hisia huwa zinapanda lakini hakuna kinachohalalisha tabia kama hiyo. Nitahakikisha haitatokea tena."