Jumatatu , 2nd Apr , 2018

Mshambuliaji wa Klabu ya Tenerife ya nchini Hispania Farid Mussa amesema kuwa yeye bado ni mchezaji wa Azam FC licha ya kuongezewa muda wa kucheza kwa mkopo kwenye klabu yake hiyo ya Hispania.

Farid Mussa ameweka wazi kuwa mkataba wa awali umemalizika mwaka huu na bado Klabu ya Azam haijamuuza hivyo bado anaendelea na mkopo lakini anaamini malengo yake yatafanikiwa.

“Mimi bado ninamkataba na Azam FC na nipo huku kwa mkopo ambao ulikuwa unaisha mwaka huu na bosi wa Tenerife aliniita na akaniambia bado tunahitaji mchango wako na wakasema wananiongeza mkataba na kama nitakubali wao wataelewana na Azam FC, ” amesema.

Farid bado anamkataba na Azam FC mpaka mwaka 2020 na anaamini ipo siku watamuuza na kuendelea na soka la kulipwa kama wachezaji wengine Wakitanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Farid ameongeza kuwa kwa sasa ameshazoea soka la Hispania na tayari ameshaanza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambayo inashiriki ligi daraja la kwanza nchini humo Segunda B.