Ijumaa , 13th Sep , 2024

Baada ya kuangalia michezo ya Al Ahly Tripoli, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema wapinzani wao wagumu sana wanapokuwa kwenye uwanja wa nyumbani na kufanyia kazi kwa ajili ya kupata matokeo mazuri katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Amesema ameona ubora na madhaifu ya wapinzani wao wanapokuwa nyumbani na anaimani mechi ya marudiano itakuwa nzuri sana Simba ikirejea Tanzania uwanja wa Benjamini Mkapa.
-
Simba wanatarajiwa kushuka dimbani Jumapili, Septemba 15 ugenini nchini Libya kuwakabili wapinzani wao hao ambapo Kocha Fadlu ameshanasa siri zao zote akisubiri tu kuwaangamiza.
-
Kocha Fadlu amesema amepata nafasi ya kuwaangalia wapinzani wao hao baadhi ya michezo yao na kubaini wachezaji wa kuwachunga hasa safu ya ushambuliaji hivyo hakuna kitakachoharibika.

“Nimeona ubora na udhaifu wa wapinzani wetu katika kila eneo ikiwemo safu ya ulinzi na ushambuliaji. Ili kupambana vema lazima umjue ndani na nje unayepambana naye na hicho ndicho ambacho tumekifanya.

“Tunakutana na timu bora ambayo msimu wa 2022 ilifika nusu fainali michuano hii ya Kombe la Shirikisho lakini tumejiandaa kikamilifu kupambana nao. Mashabiki wasiwe na wasiwasi wowote badala yake wazidishe kutuombea,” alisema Kocha huyo
-
Simba waliondoka juzi kuelekea nchini humo kwa ajili ya mchezo wao wa Jumapili dhidi ya wenyeji wao hao huku Kocha huyo akidai kuwa, wana uhakika wa kupata matokeo mazuri kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

“Hii Mechi tutaimaliza Nyumbani kwetu tutaingia kucheza kwa kuwaheshimu Tripoli kwakuwa ni timu kubwa pia wanawachezaji wazuri lakini tutapambana tupate matokeo mazuri ambayo yatatusaidia kuimaliza mechi uwanja wa nyumbani” amesema kocha huyo.
-
Baada ya mchezo huo, Simba watarejea jijini Dar es Salaam kuwasubiri wapinzani wao hao mchezo wa marudiano utakaochezwa Dimba la Benjamin Mkapa ambapo mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi ya CAFCC.