Jumapili , 12th Sep , 2021

Mcheza tenisi Emma Raducanu raia wa Uingereza mwenye miaka 18 amemaliza ukame wa Grand Slam kwa wanawake nchini Uingereza, baada ya kutwaa ubingwa wa michuano ya wazi ya Marekani (USOpen) kwa kumfunga Leylah Fernandez wa Canada kwa seti mbili za 6-4 6-3 kwenye fainali.

Emma Raducanu raia wa Uingereza akiwa na kombe la US Open

Baada kwa Emma kutwaa ubingwa huo usiku wa kuamkia leo jijini New York sasa rasmi, hii ni Grand Slam ya kwanza kwa wanawake Uingereza tangu mwaka 1977 ambapo Virginia Wade alishinda Wimbledon.

Rekodi alizoweka ni pamoja na 

1. Mwanamke wa kwanza Uingereza kushinda US Open baada ya miaka 51 mara ya mwisho alifanya hivyo Virginia Wade mwaka 1968.
2. Mchezaji aliyefuzu kwa mara ya kwanza kucheza Grand Slam na kwenda kuchukua ubingwa tena kwa kushinda mechi zote 10.
3. Mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kushinda Grand Slam tangu alipofanya hivyo Maria Sharapova kwenye Wimbledon 2004.
4. Mwanamke wa kwanza kushinda US Open bila kupoteza hata seti moja tangu alipofanya hivyo Serena Williams mwaka 2014