Jumatatu , 3rd Mei , 2021

Klabu ya Coastal Union ya Tanga kupitia kwa katibu mkuu wake Rashid Mgweno, imekanusha taarifa za kumfuta kazi kocha mkuu wa kikosi hicho Juma Mgunda na imesisitiza kuwa bado wanamipango ya muda mrefu na kocha huyo.

Kocha Juma Mgunda (katika waliosimama) akiwa na wachezaji wa Coastal Union

Katibu huyo wa Coastal Rashid Mgweno ametolea ufafanuzi taarifa za kocha Mgunda kufutwa kazi na amesema

“Hizi taarifa si za kweli na hazina ukweli hata kidogo kwa sababu ni mwalimu ambaye bado tuponaye kwenye mipango ya muda mrefu ya timu. Kwa hiyo ukinambia kwamba zimetoka taarifa tumeacha sisi wenyewe zilitushitua na ilituchanganya kwa sababu hatukujua chanzo chake kilikuwa ni nini na walikuwa na lengo gani kwenye kuzusha hizo taarifa.”

“Naomba nizikanushe hizi taarifa, na niseme Mwalimu Juma bado tupo naye na tunamkataba naye na tuna mipango naye endelevu ambayo tunaamini kabisa yeye atatufikisha ambako tunataka kufika.”

Mapema leo asubuhi zilitoka taarifa ambazo zilidai kuwa klabu hiyo ya Tanga imeachana na kocha mgunda kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo wa kikosi hicho kufuatia kuondolewa kwenye michuano ya kombe la shirikiso ya Azam Sports Federation Cup na Mwadui FC kwa kufungwa kwa mabao 2-0 katika hatua ya 16 bora.

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu wagosi wakaya wapo nafasi ya 10 wakiwa na alama 33, ikiwa ni tofauti ya alama tano kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja. Katika michezo 10 ya mwisho ya Ligi Kuu Coastal imeshinda michezo minne, imetoka sare kwenye mchezo mmoja na wamefungwa michezo mitano.