TIMU ya soka Coastal Union ya Tanga inatarajia kusheherekea miaka 53 ya Uhuru wa Tanzania kwa kucheza mechi ya kirafiki na timu ya AFC ya Arusha itakayochezwa kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani Desemba 9 mwaka huu.
Mechi hiyo ni maandalizi kwa timu hiyo kujiandaa na mechi zake za Ligi kuu soka Tanzania bara baada ya mapumziko ya siku kumi kutokana na Ligi kuu kusimama kwa muda ambapo itaendelea Desemba 26 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,Ofisa Habari wa Coastal Union,Oscar Assenga amesema kuwa mechi hiyo itakuwa ni muhimu kwa timu hiyo kujitayarisha kwa ajili ya raundi inayofuata kwenye michuano hiyo.
Amesema kuwa baada ya kumalizika mechi hiyo wataangalia uwezekano wa kutafuta mechi nyengine ya majaribio kabla ya kuanza ligi hiyo ambayo msimu huu imeonekana kuwa na upinzani mkubwa
Aidha amesema kuwa timu hiyo ya AFC yenye makazi yake Mkoani Arusha inatajiwa kuwasili mkoani Tanga Desemba 8 mwaka huu kwa ajili ya mtanange huo lengo likuwa kuziandaa timu zote mbili kwa mashindano yanayowakabili.
Amesema kuwa mechi hiyo ina umuhimu kwa timu zote mbili sisi ni kujiandaa na Michuano ya Ligi kuu Tanzania bara raundi inayofuata na wapinzania wetu wanajiandaa na Ligi daraja la kwanza hapa nchini.
Hata hivyo amesema kuwa mazoezi ya timu hiyo yameendelea kushika kasi kwenye viwanja vya Mkwakwani mjini Tanga baada ya wachezaji wote waliokwenda mapumziko kurejea kwa asilimia kubwa.