Ijumaa , 13th Jan , 2023

Todd Boehly anakaribishwa kwenye ulimwengu wa 'stress', licha ya pesa zake zote lakini moja ya kitu kinamnyima usingizi hivi sasa ni Chelsea, usajili bora anaendelea kuufanya lakini matokeo bado magumu, hiki kitu huwa kinawapa shida sana matajiri hasa kwenye biashara zao.

Kocha wa Chelsea, Grahm Potter na nahodha Cesar Azpilicueta

Mashabiki wengi wa Chelsea wanaamini angekuwepo bosi Roman Abramovich asingekubali kudhalilishwa namna hii. Wanakumbuka urejeo wa pili wa Jose Mourinho pale darajani, alishinda ubingwa wa ligi lakini baada ya mechi 18 za msimu uliofuata, Roman Abramovich akamla kichwa kabla ya sikukuu ya Christmas 2015 kwasababu yeye alikuwa mtu wa matokeo na ndiyo maana Chelsea imekuwa kubwa na kufikia hapa ilipo kuwa na mataji 2 ya Klabu Bingwa Ulaya kuizidi Arsenal na taji moja nyuma ya Man United.

Kama hiyo haitoshi msimu 2016/17 Chelsea ilishinda ubingwa wa EPL na FA Cup chini ya Antonio Conte, halafu niulize nini kilitokea msimu uliofuatia!!. Conte alitimuliwa kwa kuikosesha Chelsea nafasi ya kushiriki Klabu Bingwa Ulaya.

Kwenye miaka takribani 19 ya Abramovich pale Chelsea ameajiri makocha 13, lakini ndiyo timu yenye mafanikio makubwa ya ndani na nje, kutokana na mtazamo tu wa Abramovich. Bwana Todd Boehly  ameamua kuja na mfumo tofauti wa kuamini mipango ya muda mrefu, ndiyo maana hata bodi yake imekuja na kauli ya kumlinda kocha Graham Potter licha ya matokeo mabaya anayopitia.

Lakini tunamkumbusha kuwa hakuna kocha Muingereza aliyechukua ubingwa wa EPL tangu Sir Alex Ferguson alipofanya hivyo mwaka 2013. Ni yeye tu bwana Boehly kuamua 'Punda afe mzigo ufike' ili mashabiki waendelee kula burger au kuwa baridi kusubiri project ambayo itazaa matunda baada ya miaka kadhaa huku akiwalisha kisamvu cha kwetu Nakapanya !!

Imeandikwa na @manafi_daimu