Jumapili , 27th Aug , 2017

Aliyekuwa mgombea wa urais ambaye pia ni mwanasheria kitaaluma Hashim Rungwe Spunda, ameitaka serikali kufanya uchunguzi wa tukio la milipuko lililoteketeza ofisi za mawakili wa IMMMA, na kusema ni tukio la kigaidi lenye kuleta hofu.

Hashim Rungwe Spunda

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mh. Hashim Rungwe amesema tukio hilo si jambo zuri kwa jamii hivyo ni muhimu serikali chini ya vyombo vyake vya usalama vifanye uchunguzi wa kina, ili kuweza kubaini kwa nini ofisi hizo zimeteketezwa, kwa tukio linalotia hofu wananchi.

Inaleta hofu, huu ni mtindo wa ugaidi, sasa watu watakuwa wanaogopa na kuogopa hakusaidii, si jambo jema kama ni kweli na sasa kwa sababu ni mapema mno kuanza kulijadili, tuviachie vyombo vya ulinzi na usalama tujue vitasema nini, lakini ni jambo hili limetuhuzunisha sana sote, na kwa bahati nzuri hakukutokea maafa, lakini ni jambo baya na nafikri lifanyiwe utafiti wa kutosha", alisema Hashim Rungwe.

Hashim Rungwe aliendelea kwa kusema kuwa iwapo serikali haitafanya hivyo itaweka hali ya sintofahamu na kubeba lawama juu ya tukio hilo, kutokana na kile alichokieleza kwamba ofisi hiyo ni ya mawakili wanaowakilisha wafanya biashara ambao wana mgogoro na serikali.

"Hili jambo kama kweli ni bomu basi tunaomba vyombo husika vifuatilie sana, wafuatilie wajue kitu gani kinatokea, na kwa nini iwe kwenye ofisi ya wale, na wale tunasikia wanawakilisha wafanya biashara fulani fulani ambao wengine wana ugomvi na serikali, sasa watu wanaweza wakajenga fikra kwamba kwa namna moja au nyingine wanahusika na mambo haya, lakini kwa sababu tuna vyombo vya usalama vifanye utafiti wa kutosha tujue nani anahusika na mambo haya", alisema Hashim Rungwe.

Ofisi ya za mawakili wa IMMMA zilizopo Upanga jijini Dar es Salaam zimeungua moto usiku wa Ijumaa, huku chanzo cha moto huo kikielezwa ni milipuko, na mpaka sasa waliohusika na tukio hilo bado hawajafahamika.

Msikilize Hashim Rungwe hapa chini akizungumzia tukio hilo.