Jumanne , 10th Oct , 2017

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeomba kukutana na shirikisho la soka nchini kwaajili ya kujadili namna nzuri ya kufanya maboresho ya viwanja vinavyomilikiwa na Chama hicho Tawala.

Hilo limethibitishwa leo na Afisa habari wa TFF Alfred Lucas ambapo ameeleza kuwa CCM imeomba kukutana na viongozi wa TFF ili kujadili kuhusu uboreshaji wa viwanja vinavyomilikiwa na Chama hicho.

“CCM imeomba kukutana na TFF ili kuona njia sahihi ya kuboresha viwanja kama unavyojua asilimia kubwa ya viwanja nchini vinamilikiwa na Chama Tawala”, amesema Alfred Lucas.

Aidha Lucas amepongeza kuwa lengo kuu ni kuboresha miundombinu ya soka nchini hivyo TFF kupitia watalaam wake wa viwanja watashauriana na CCM ili kufikia malengo.

Moja ya uwanja mkubwa ambao unamilikiwa na Chama cha Mapinduzi ni CCM Kirumba uliopo jijini Mwanza wenye uwezo wa kuingiza mashabiki zaidi ya elfu 45.