Camelo Anthony kuweka historia ya kibabe NBA ?

Jumatatu , 3rd Mei , 2021

Nyota wa timu ya kikapu ya Portland Trail Blazers, Camelo Anthony huenda akaingia kwenye orodha ya kumi bora ya wana kikapu wenye alama nyingi kwenye historia ya Ligi ya hiyo nchini Marekani atafanikiwa kupata alama 23 dhidi ya Atalanta Hawks usiku wa kuamkia kesho.

Nyota wa timu ya kikapu ya Portland Trail Blazers, Camelo Anthony.

Camelo mwenye misimu 18 ya NBA, kwasasa anashika anafasi ya 11 kwenye orodha ya wana kikapu wenye alama nyingi kwenye historia ya NBA akiwa na alama 27, 303 na akifanikiwa kupata alama 23 basi atampiku Elvin Hayes aliyepo nafasi ya kumi akiwa na alama 27, 313. 

Kinara wa kuvuna alama nyingi ni gwiji wa mchezo huo, nyota wa zamani wa Milwaukee Bucks na Los Angeles Lakers, Kareem Abdul-Jabbar mwenye alama 38, 387 akifuatiwa na nyota wa zamani wa Utaj Jazz na Los Angeles Lakers, Karl Malone mwenye alama 36,928.

Lebron James ambaye kwa sasa anakipiga kwenye timu ya Los Angeles Lakers anashika nafasi ya tatu akiwa na alama 35,299 na kumuacha mbali Camelo Anthony anayelazimika kuvuna alama 11, 084 kumfikia kinara Jabbar na alama 7,996 kumfikia Lebron ambaye bado anacheza.

Mbali na mchezo wa Portland dhidi ya Atalanta, NBA itaendelea leo kwa michezo mingine 7 ambapo, mabingwa watetezi LA Lakers watakuwa na kibarua kigumu mbele ya Denver Nuggets wakati Sun Antonio Spurs watacheza na Utah Jazz vinara wa magharibi saa 11:00 Alfajiri kesho.

Vinara wa upande Mashariki, Philadelphia watakipiga na Chicago Bulls saa 11:00 alfajiri pia, wakati ambao New Orleans Pelicans watachuana na Golden State Warriors saa 8:30 usiku wa kuamkia kesho.