
Mwamuzi Aden Marwa, aliyefungiwa maisha na CAF kujihusisha na masuala ya soka
Kifungo hicho kimekuja baada ya filamu iliyorekodiwa na mwandishi wa habari za kiuchunguzi, Anas Amerayan Anas ikimuonesha akipokea fedha siku chache kabla ya kuanza kwa michuano ya kombe la Dunia nchini Urusi.
Marwa ambaye alichaguliwa na FIFA kuchezesha michezo ya kombe la Dunia, aliondolewa katika listi baada ya mwandishi huyo kuweka hadharani ripoti yake ya uchunguzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, Jumla ya waamuzi 22 wameadhibiwa wakiwemo Yannisou Bebou raia wa Togo na Jallow Ebrima raia wa Gambia ambao wamefungiwa kwa miaka 10 kila mmoja.
Wengine waliokubwa na rungu la CAF ni makamisaa wa mchezo wapatao Saba ambao wamesimamishwa kwa kipindi cha miaka miwili hadi mitano na wengine 11 wakiamuliwa kuhudhuria katika kikao cha kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo, August 5.
Mwezi uliopita, Rais wa zamani wa shirikisho la Soka la Ghana (GFA), Kwesi Nyantakyi alijiuzulu nafasi yake ya umakamu wa kwanza wa Rais wa CAF kutokana na tuhuma hizohizo za rushwa.