
Shirikisho la soka Tanzania TFF limesema litaendelea kuipa kipaumbele timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars katika kufanya maandalizi yake licha ya kuvurugika kwa ratiba ya ligi kuu nchini inayoendelea hivi sasa.
Mkurugenzi wa bodi ya ligi Boniface Wambura amesema kuwa tayari wamepokea maombi kutoka benchi la ufundi la Stars linalohitaji siku 10 za maandalizi kabla ya mechi ya kufuzu kucheza kombe la dunia mwaka 2018 dhidi ya Algeria mwezi ujao.
Wambura amesema mabadiliko kunako ligi kuu ya soka Tanzania bara yataendelea kujitokeza ili kuipa nafasi timu ya taifa ambayo inakabiliwa na mechi mbalimbali za kimataifa ikiwemo dhidi ya Algeria na michuano ya Challenge itakayoanza kutimu avumbi hivi karibuni.
Wakati huohuo katika kuhakikisha inafanya vema kunako mashindano mbalimbali ikianzia mechi ya Novemba 14 dhidi Algeria Rais wa TFF Jamali Malinzi ameunda kamati maalum itakayoitwa ya Kamati ya Taifa Stars.
Malinzi amesema majukumu ya kamati hiyo ni kuimarisha huduma kwa wachezaji,uhamasishaji masoko,kuhamasisha wachezaji na kuandaa kusimamia mikakati ya ushindi.
Wajumbe wanaounda kamati hiyo walioteuliwa na Rais Malinzi, ni Farouck Baghouza ambaye ni mwenyekiti, Katibu ni Teddy Mapunda.
Wajumbe ni Juma Pinto, Michael Richard wambura,Iman Omar Madega,Salum Abdallah na Isaac Chanji.