Biashara United mzigoni leo kombe la Shirkisho CAF

Ijumaa , 10th Sep , 2021

Klabu ya Biashara United Mara kutoka mkoani Mara inataraji kushuka dimbani saa 12:00 Jioni ya leo Septemba 10, 2021 ugenini dhidi ya Dikhil ya nchini Djibout kwenye uwanja wa 'Stade De Vulle' kwenye mchezo wa hatua ya awali ya mtoano kuwania kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kikosi cha Azam kikiendelea na Mazoezi (juu kushoto), Yanga nao wakiwa mazoezini (chini kushoto) na kikosi cha Biashara United Mara kabla ya kucheza moja ya mchezo wake wa kirafiki.

Biashara United Mara ambayo inataraji kucheza michezo ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza tokea kuanzishwa kwa klabu hiyo miaka 8 iliyopita, iliondoka mchini usiku wa kuamkia leo kuelekea nchini Djibout kwa kupitia nchini Ethiopia baada ya jana kukwama uwanja wa ndege wa kimataifa wa JK Nyerere kwa sababu baadhi ya wachezaji wake kutokamilisha taarifa za kusafiria.

Kwa upande mwingine, Klabu ya Azam imethibitisha kukamilisha maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Horseed ya Somalia wa hatua ya awali ya mtoano kuwania kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Chamazi jijini Dar es Salaam saa 1:00 usiku wa   kesho Jumamosi ya Septemba 11, 2021.

Azam itacheza mchezo huo bila ya mfungaji wa klabu hiyo wa msimu uliopita, Prince Dube ambaye jana Septemba 9, 2021 amefanyiwa upasuaji salama katika hospitali ya Vicent Pelloti jijini Cape Town, Afrika Kusini na sasa hali yake ni nzuri na Jumatatu Septemba 13 atarejea nchini.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Azam, Zacharia Thabiti amesema Dube alikuwa anapata maumivu makali kwenye maeneo la chini ya kitovu kushoto pindi akaijaribu kukimbia kwa kasi hivyo wanaimani tatizo hilo litapona na Dube kurejea kwenye utimamu wake wa kawaida.

Kwa upande wa mwakilishi mwingine wa Tanzania kwenye michezo ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa Afrika ni Yanga ambao wanaratiba ya kukipiga dhidi ya Rivers United ya Nigeria saa 11:00 jioni kwenye dimba la BW Mkapa kukiwa na tamko la CAF kuzuia watazamaji kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo kutokana na uwepo wa Covid-19.

Kuelekea kwenye mchezo huo, Msemaji wa Yanga, Haji Manara amethibitisha leo Septemba 10, 2021 kuwa bado hawajapokea barua ya majibu kutoka CAF juu ya hati za usajili wa kimataifa kwa wachezaji wao Djuma Shabani, Fiston Mayele na Khalid Aucho hivyo hawatokupewo kwenye mchezo huo siku ya Jumapili hii.

Manara alishawatoa shaka wanayanga kwa kusema, Yanga ni timu kubwa hivyo imesajili wachezaji wengi pamoja na waliopo hivyo wanauwezo wa kucheza na Rivers United bila ya uwepo wa nyota hao watatu licha ya kukiri watatu hao ni wachezaji wenye uwezo mkubwa sana kuisaidia Yanga kimataifa.