Ijumaa , 1st Feb , 2019

Kwa mujibu wa ripoti ya kiutafiti ya Septemba 2018 ya mtandao wa Sportskeeda, Chelsea imeongoza kuwa ni klabu pekee barani Ulaya iliyokuwa na wachezaji wengi waliowatoa kwa mkopo vilabu mbalimbali.

Michy Batshuayi

Jumla ya wachezaji 29 wametolewa kwa mkopo na klabu hiyo, akiwemo mshambuliaji aliyeng'ara katika Kombe la Dunia na timu ya taifa ya Ubelgiji, Michy Batshuayi.

Tukimzungumzia Batshuayi ni mchezaji ambaye Chelsea inamuhitaji na wakati huohuo haimuhitaji kutokana na namna ambavyo imekuwa ikimzungusha katika vilabu mbalimbali kwa mkopo tangu mwaka 2016 alipojiunga na klabu hiyo akitokea Olympic Marseille ya Ufaransa.

Baada ya kujiunga na Chelsea msimu wa 2016/17, Batshuayi alicheza michezo 32 pekee, akifunga mabao 19 kabla ya kupelekwa kwa mkopo katika klabu ya Borussia Dortmund mwezi Januari mwaka 2018. Akiwa Dortmund alionesha kiwango kizuri kwa muda mfupi, ambapo alicheza mechi 10 na kufunga mabao 7 kabla ya kukumbwa na majeraha.

Dortmund ilimrudisha Chelsea mwishoni mwa msimu wa 2017/18 na hatimaye Chelsea kumtoa tena kwa mkopo katika klabu ya Valencia ambapo aliishia kucheza mechi 15 na kufunga bao moja pekee. Kutokana na kiwango kibovu, klabu hiyo imetangaza kutoendelea naye na kumrejesha Chelsea ambako jana limetangazwa dili lingine la kujiunga kwa mkopo kunako klabu ya Crystal Palace.

Kwa mazingira hayo yote, inaonekana kabisa kuwa Chelsea haitaki kumuuza mchezaji huyo lakini wakati huohuo haiko tayari kumpa nafasi nyingine ya kujaribu katika kikosi cha kwanza, kwani ingelikuwa na nia hiyo isingemsajili mshambuliaji Gonzalo Higuain kwa mkopo kutoka AC Milan kwaanjili ya kuimarisha safu ya ushambuliaji.