Jumatano , 29th Jun , 2016

Klabu ya soka ya Chelsea ipo mbioni kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Ubelgiji Mitchy Batshuay baada ya kuripotiwa kuwa ofa yao ya pauni milioni 33 imekubaliwa na Marseille.

Mitchy Batshuay anayetajwa kukaribia kutua Stanford Bridge.

Batshuay amekua mhimili mkubwa katika klabu yake ya sasa ya nchini Ufaransa ambapo msimu uliopita aliipachikia mabao 17 katika mashindano yote.

Nyota huyo ambaye kwa sasa yupo nchini Ufaransa na timu yake ya Taifa ya Ubelgiji wakishiriki michuano ya mataifa ya Ulaya amekua akihusishwa na kutaka kuhamia katika klabu za West Ham United na Crystal Palace zote za Uingereza.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 22 alishindwa kutokea kwenye mkutano wa timu yake ya taifa na waandishi wa habari uliofanyika leo huku ikisemekana kukosekana kwake ni kutokana na kuhitajika kwake na klabu ya Marseile ambao walimhitaji kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo ya uhamisho wake.

Nyota huyo huenda akawa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na kocha mpya wa Chelsea Antonio Conte ambaye kwa sasa yupo na timu ya Taifa ya Italia huko nchini Ufaransa katika michuano ya Mataifa ya Ulaya yanayoendelea kushika kasi yake.