
Mwenyekiti wa baraza la wadhamini la Yanga, Kapt (Mst) George H. Mkuchika
Maamuzi hayo yameelezwa katika mkutano na wanahabari uliofanyika makao makuu ya klabu hiyo, ambapo kwa pamoja baraza hilo la wadhamini limeridhia kurejea kwa mwenyekiti huyo wa klabu.
Akizungumza kuhusu hilo, Mwenyekiti wa baraza la wadhamini la Yanga ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika amesema,
"Kwenye mkutano mkuu ule wa wanachama, ilipigwa kura nani wanamtaka Manji arudi, wajumbe wote 4500 walisema tunamtaka Manji arudi na sisi katika baraza la wadhamini tukasema Manji aandikiwe barua ", amesema.
"Tukamuandikia barua na mimi mwenyekiti wa baraza ndiye niliyetia saini, amejibu Manji kwa kifupi anasema, "Nimepokea maamuzi ya wanachama wa Yanga, lakini bahati mbaya kipindi nimepokea nipo kwenye matibabu, tarehe 15 Disemba madaktari wanasema nitakuwa nimekamilika, nitaanza kuhudhuria ofisini mara kwa mara kuanzia 15, Januari," ameongeza Mkuchika.
Pia, Mkuchika amesema kuwa klabu hiyo sasa ina mwenyekiti wake ambaye ni Yussuph Manji na suala hilo liko kihalali kwakuwa ni maamuzi ya mkutano mkuu.
Maoni mengine ambayo baraza la wadhamini imekubaliana ni pamoja na kuiagiza kamati ya utendaji ya Yanga kukaa meza moja na TFF ili kujadili juu ya kujaza jina la Yussuph Manji katika majina ya wagombea pamoja na kusuala la kusimamia uchaguzi wa klabu hiyo, ikitaka uchaguzi usimamiwe na kamati ya uchaguzi ya klabu badala ya TFF.