Kocha wa Mchenga (wa kwanza kushoto), MVP Baraka Sadick (wa tatu kutoka kulia) wakiwa na baadhi ya mashabiki
Ameyasema hayo katika kipindi cha Dadaz kinachoruka kupitia EATV, ambapo amesema kuwa anamfahamu vizuri Baraka Sadick tangu akiwa kijana mdogo kipindi alipokuwa akija katika mazoezi yake.
"Awali kabisa wakati mimi nacheza kikapu, wao (Baraka na wenzake) walikuwa wanakuja wakiwa wadogo wananiona nacheza, tukishamaliza na wao wanaingia uwanjani wanarusha mipira. Nimekuwa mfano bora kwake, simaanishi nimehusika asilimia 100 lakini nimemfundisha", amesema Mudi.
"Kina Baraka hawawezi kuondoka Mchenga kwa sababu mimi nipo, hiyo ipo hata kwa Tamaduni kuna watu wa aina hiyo, mfano yule Stefano wa Tamaduni niliwahi kumfuata akaniambia subiri baada ya wiki na hatimaye siku zikapita nyingi mwisho akaniambia siwezi kuacha hapa na mimi nikamuelewa", ameongeza.
Akizungumzia ushindani aliokutana nao dhidi ya Taamaduni na fainali ngumu kwake, Mudi amesema, "katika game za fainali mwaka huu dhidi ya Tamaduni, game ya kwanza ndiyo ilikuwa hatari zaidi kwetu, walikuwa na nafasi ya kushinda. Tulikuwa tukiwazidi wanarudisha ilikuwa ngumu sana".
Mchenga wameshinda ubingwa baada ya kushinda michezo mitatu ya fainali dhidi ya Tamaduni, na kujishindia kitita cha Sh. milioni 10 na Tamaduni wakijishindia Sh. milioni 3. Mchezaji Baraka Sadick ameshinda tuzo ya MVP kwa msimu wa pili mfululizo na kujishindia Sh. milioni 2.