Azam FC walipofanya mazoezi ya mwisho hapo jana katika Uwanja wa Olympique de Rades utakapofanyika mchezo leo dhidi ya Esperance.
Msemaji wa Azam FC Jaffery Iddy Maganga amesema, kikosi kipo kamili kwa ajili ya kuweza kupata ushindi katyika mchezo huo japo wanaamini utakuwa mgumu kutokana na timu wanayokutana nayo kuwa nzuri.
Maganga amesema, kikosi cha Azam FC kinaamini maandalizi mazuri yatasaidia kuweza kupata ushindi na kuweza kusonga mbele katika michuano hiyo.
Daktari wa Azam FC Juma Mwimbe amesema, majeruhi watatu ndio hawataonekana kabisa katika mchezo huo ambao wamebaki jijini Dar es salaam wakiwemo Shomary Kapombe, Paschal Wawa na Kipre Tchetche huku Farid Mussa ambaye alikuwa majeruhi akiwa na silimia zote za kuweza kucheza mchezo huo kutokana na hali yake kuendelea vizuri.
Kwa upande wake Didier Kavumbagu amesema, wanaamini wanakutana na timu kubwa lakini haiwaogopeshi na kila mchezaji atakayepangwa anatakiwa kuziba pengo la ambao hawapo na kuonyesha uwezo ili kuipa timu ushindi.
Kwa upande wake Ramadhan Singano amesema, wachezaji wote wamejiandaa vizuri kwa ajili ya kupambana na hawana wasiwasi kwani kila mchezaji anajua nafasi yake na anatakiwa ni kitu gani afanye katika mchezo huo.
Azam FC inahitaji ushindi wowote au sare yoyote ili kusonga mbele kutokana na ushindi wa mabao 2-1 walioupata jijini Dar es Salaam wiki moja iliyopita.