
Katika michezo iliyopigwa hapo jana Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, bao pekee la Mganda Hamisi Kizza ‘Diego’ limeipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga huku mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Bakari Kigodeko akiipokonya tonge mdomoni Yanga SC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga baada ya kuifungia Mwadui FC bao la kusawazisha dakika la salama timu hizo zikitoka sare ya 2-2.
Kwa matokeo hayo Yanga inaendelea kuwa kileleni mwa Ligi kwa kuwa na Pointi 20 baada ya jana kugawana Pointi moja moja na Mwadui ikifuatiwa na Azam Fc yenye Pointi 19 ambao leo hii wanashuka kutafuta Pointi tatu na ikiibuka na ushindi itakaa kileleni na kuishusha Yanga Sc huku Simba wakiwa na Pointi 18.
Matokeo mengine ya hapo jana huko Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Toto African imeweza kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo huku wakata miwa wa Turiani, Mtibwa Sugar wakiwakalisha ndugu zao Kagera Sugar kwa bao 1-0 Uwanja Manungu Complex mkoani Morogoro, Ndanda FC wakitoka sare ya bila kufungana na Stand United uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Mbeya Citu wakitoa sare ya bao 1-1 na Majimaji Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya