Jumanne , 1st Mar , 2022

Ligi Kuu ya NBC Tanzania inataraji kuendelea tena leo Jumanne Machi 1, 2022 kwa mchezo mmoja ambapo Azam FC watakuwa wenyeji wa Coastal Union wagosi wa kaya saa 1:00 usiku kwenye dimba la Chamazi.

(Rodgers Kola akishangilia baada ya kufunga moja ya bao kwenye Ligi kuu)

 

Kuelekea kwenye mchezo huo, Kocha msaidizi wa Azam FC John Matambala amethibitisha kuwa, inataraji kuwakosa wachezaji wake watano kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo majeraha.

Wachezaji hao watakaokosekana ni washambuliaji wanne, Iddy Suleimani Nado mwenye majeraha ya muda mrefu, Idriss Mbombo aliyeumia mazoezini, Shaban Iddy Chilunda, Rodger Kola mwenye kadi tatu za njano na beki Nicholas Wadada.

Kwa upande wa Coastal Union, Kocha wake Joseph Lazaro amesema maandalizi yao yanaendelea vizuri huku wakitaraji kumkosa mchezaji mmoja pekee kwa kuoneshwa kadi na si kwa kuwa na majeraha.

Mchezo huo unatazamiwa kuwa ni wa 18 tokea Septemba 21, 2011 ambapo Azam FC ameibuka mbabe kwakupata ushindi kwenye michezo 9, Coastal Union ikishinda michezo 4 na kutoa sare 4.

Mara ya mwisho Coastal Union kuifunga Azam FC ilikuwa Februari 15, 2020 kwa mabao 2-1 mchezo ambapo pia ilikuwa ni kwa mara ya kwanza Coastal Union kupata ushindi kwenye dimba la Chamazi Jijini Dar es Salaam.

Azam FC ipo nfasi ya tatu, ikiwa na alama zake 24 wakati Coastal Union ipo nafasi ya 11 ikiwa na alama zake 17.