Jumanne , 3rd Mei , 2016

Kipa David De Gea ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Manchester United kwa mara ya tatu mfululizo baada ya Jumatatu usiku kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa klabu hiyo.

Golikipa wa klabu ya Manchester United David de Gea

De Gea ametwaa tuzo hiyo maarufu kama 'Matt Busby Player of the Year' ikiwa ni baada ya kutoruhusu kufungwa bao lolote katika michezo 14 kati ya 32 ya Ligi Kuu England aliyoicheza Manchester United msimu huu wa 2015/2016 huku pia akifanya vizuri katika michuano ya kombe la FA.

Mbali ya De Gea nyota mwingine aliyewahi kutwaa tuzo hiyo kubwa zaidi mara tatu lakini katika vipindi tofauti ni Mreno Cristiano Ronaldo. Ronaldo alitwaa tuzo hiyo mwaka 2004, 2007 na 2008.

Baada ya kutwaa tuzo hiyo De Gea alisema ni vigumu kusema chochote kwani kutwaa tuzo hii mara tatu mfululizo ni faraja na heshima kubwa kwake.

Wengine walioshinda tuzo usiku wa Jumatatu ni: Chris Smalling aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka chaguo la wachezaji (United’s Players’ Player of the Year), Cameron Borthwick-Jackson aliyetwaa tuzo ya mchezaji wa mwaka kwa wachezaji wa U-21(Under-21 Player of the Year) huku Marcus Rashford akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwa wachezaji wa U-18 (Under-18 Player of the Year).