wanafunzi wa Turiani wakifurahi baada ya kukabidhiwa taulo za kike za mwaka mzima.
Wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu wapatao 59 wamepatiwa pakiti 716 za taulo za kike zitakazowasaidia kutumia kwa mwaka mzima.
Mratibu wa Kampeni ya Namthamini, Millicent Lema Lasway amesema lengo la kampeni hiyo kufika katika shule hiyo ni kutoa elimu ya hedhi, ambayo ni lazima itolewe kwa watoto wa kike na kiume, na ikiwa ni siku ya Mtoto wa Afrika Duniani ni vyema kuvunja ukimya na kutoa elimu ya afya kwa watoto.
''Tunashukuru kuona watoto wa kiume wamejitokeza, kwa sababu kampeni yetu licha ya kumsaidia mtoto wa kike pia inalenga kuvunja ukimya juu ya hedhi.'' alisema Millicent Lasway
''Maisha yanabadilika na vijana tunajifunza vitu vingi, sio kitu cha ajabu ndiyo maana tukapenda watoto wa kiume wawepo" aliongezea Millicent Lwasay
Pia Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Turiani, Projestus Barongo amaeiomba serikali kuondoa kodi katika taulo za kike ili kuwawezesha watoto wa kike kuwa huru wawapo katika siku za hedhi.
Kampeni ya Namthamini imeingia msimu wa sita mwaka huu, zoezi la uchangiaji linaendelea na wadau wanaombwa kuchangia kampeni hii ili kusaidia na kuinua kiwango cha elimu nchini kwa watoto wa kike ambao hukosa masomo kwa zaidi ya siku 50 kwa mwaka.
Hii ni shule ya tano iliyofikiwa na Kampeni ya Namthamini tangu izinduliwe Mei 27 mwaka huu.