
Sultan wa Oman Qaboos bin Said
Kupitia EATV & EA Radio Digital, tumekuandalia historia fupi ya maisha ya Sultan Qaboos bin Said na ugonjwa ulioutoa uhai wake.
Maisha yake ya awali
Kiongozi Sultan Qaboos bin Said amezaliwa Novemba 18, 1940 na kufariki Januari 10, 2020, amekaa madarakani kwa muda wa miaka 50, alianza kuiongoza Oman mwaka 1970 hadi umauti unamkuta alikuwa yupo katika uongozi.
Ameweka rekodi ya kukaa madarakani kwa muda mrefu katika nchi za Mashariki ya kati hadi kwenye nchi za falme za kiarabu.
Maisha Binafsi
Sultan Qaboos Bin Said ni mtoto pekee katika uzao wa baba yake ambaye alikuwa kiongozi wa Oman aitwaye Sultan Said bin Taimur na mama yake Sheikha Mazoon al-Mashani, alioa wake watatu katika nyakati tofauti na katika maisha yake hajawahi kupata mtoto wala ndugu wa kuzaliwa naye tumbo moja.
Elimu
Elimu ya msingi na sekondari alipata katika shule ya Salalah, kisha akahamishiwa shule binafsi ya St Bury St Edmunds nchini Uingereza akiwa na umri wa miaka 16, alivyofikisha miaka 20 alijiunga na chuo cha ufalme wa kijeshi na alipohitimu kozi hiyo mwaka 1962 alijiunga katika jeshi la Uingereza.
Ugonjwa na Kifo
Kuanzia mwaka 2015 alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya Saratani ya utumbo mpana "Colon Cancer", hadi kufikia Disemba 14,2019 kutoka katika hospitali ambayo ilikuwa inampa matibabu UZ Leuven nchini Ubelgiji, ilitangaza kuwa hatachukua muda mrefu wa kuishi duniani, ambapo yeye mwenyewe alitaka arudishwe nyumbani ili umauti ukimfika umkutie akiwa kwao.