Jumatatu , 28th Jan , 2019

Muigizaji mkongwe nchini Salome Nonge (Mama Abdul) ameacha wosia kwa ndugu zake, ambao walikuwa wakimuuguza mpaka mauti yalipompata nyumbani kwake Mburahati jijini Dar es salaam.

Mama Abdul enzi za uhai wake.

Baba mdogo wa marehemu mama Abdul amesema enzi za uhai wake muigizaji huyo aliagiza kuwa endapo akifariki, basi ndugu zake wasiruhusu yeye kupelekwa kuagwa katika viwanja vya 'Leaders Club'.

"Sisi ma 'star' mara nyingi tukifariki huwa tunapelekwa viwanja vya 'leaders' ili kuagwa na mashabiki kutoka pande zote za jiji la Dar es salaam, lakini mimi naomba mnipeleke kanisani na wanaonipenda wote watakuja kanisani", maneno ya mama Abdul.

Baada ya baba mdogo kuhoji kwanini aliamua hivyo, alimjibu kuwa, "Sihitaji mtumie gharama kubwa na kutembezwa kwa umbali mrefu kutoka Leaders hadi kunirudisha makaburi ya Chang'ombe".

Mama Abdul amefariki dunia Ijumaa ya Januari 25, nyumbani kwake maeneo ya Mburahati jijini Dar es salaam ambapo alizidiwa ghafla. Alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa homa ya Ini, na atazikwa leo mchana katika Makaburi ya Chang'ombe.