Jumanne , 21st Jun , 2016

Msanii ambaye pia ni Mfalme wa mashairi hapa Bongo katika muziki wa Hip Hop, Selemani Msindi aka Afande Sele, amesema wasanii wa bongo sasa hivi hawana ubunfu kabisa, na badala yake wanatumia kiki kujitangaza.

Akiongea kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Afande Sele amesema zamani walikuwa wanatumia rushwa na kujuana ili kuweza kupata air time kwenye vituo vya radio na runinga, lakini sasa wasanii wanatumia skendo ili kujitangaza katika kazi zao.

"Watu wamekosa ubunifu kwenye kazi zao, ile hatahari ambayo tulikuwa tunaiona siku za nyuma sasa hivi ndio inajidhihirisha zaidi, watu walikuwa wanapata air time kwa ajili ya rushwa, kujuana, lakini walikuwa hawana ubunifu, kwa hiyo sasa hivi wameamua kutumia kiki za mambo ya mapenzi, kwa vile tayari uwezo wao wa kubuni na kusababisha watu wawakubali moja kwa moja kupitia kazi zao unakuwa hakuna," alisema Afande Sele.

Afande Sele amesema kitendo hicho sio kizuri kisipodhibitiwa, kwani kinachangia kwa kiasi kikubwa kuua muziki wa Bongo fleva, kwani watu wameshindwa kabisa kuandika mashairi mazuri yenye ujumbe.

"Mtu anakuwa hana uwezo wa kuonyesha uwezo wa kipaji chake moja kwa moja ili kazi zake zisikike lazima atafute namna nyingine ya kusikika na kuonekana, na ndio hiyo kamchukua fulani, mara kazaa na fulani, mara anataka kumuoa fulani, watu wameshindwa kutunga, wameshindwa kushawishi watu," alisema Afande Sele.