Ijumaa , 6th Mar , 2020

Kupitia show ya PlanetBongo ya East Africa Radio, Meneja wa msanii Alikiba aitwaye Esi Mgimba, amesema sababu ya msanii wake kufanya kazi na watoto wa kike ni idadi ya mashabiki wengi wa kike alionao hapa nchini.

Alikiba na Meneja wake Esi Mgimba

Akizungumza hayo kuelekea siku ya mwanamke duniani, ambapo East Africa TV pamoja na Radio wanaiita MwanamkeKinara, Meneja huyo amesema anajivunia kufanya kazi na Alikiba ambaye amefanya kumkutanisha na watu wengi ambao hakutegemea kukutana nao.

"Mimi ni mtoto pekee kwa mama yangu, japo kwa upande wa baba nilikuwa na ndugu wengine, nilikuzwa na mama pekee nilimuona akipambana na akihakikisha nipo sehemu fulani, kwahiyo mama yangu ndiyo kinara wangu" amesema Meneja wa Alikiba.

"Kuhusu Alikiba sijui kwanini huwa anaamua kufanya kazi na wanawake, ila naamini mziki wake unasikilizwa na watu wengi, lakini asilimia kubwa ni idadi ya wadada, na najivunia kufanya naye kazi" ameongeza.

Aidha akiwazungumzia wanawake kuelekea katika siku ya wanawake duniani amesema, "Katika vitu vinavyonipa wakati mgumu kwa sasa ni jinsi mitandao ya kijamii inavyoharibu ndoto za watoto wa kike wengi, natamani sana itolewe elimu ya mitandao hasa kwa mabinti".