Jumatatu , 19th Feb , 2018

Mchekeshaji maarufu na mwenye umri mdogo zaidi kutokea nchini Nigeria Emanuella Samuel amepata 'shavu' jipya la kufanya kazi na kampuni kubwa dunia ya utengenezaji filamu ya Disney Studios.

Hayo yamebainishwa na Emanuella mwenyewe kutumia ukurasa wa kijamii anaoutumia kwa kuweka picha zenye ujumbe wa kuwashukuru watu wa karibu walioweza kumpa ushirikiano muda wote.

"Asanteni Disney Studios, Mungu awabariki watu wote mlionipa ushirikiano mpaka kufika hapa. Sikuwahi kuota kuwa hapa. Sikuwa na ndoto ya kuwa hapa mapema hivyo, nina shauku na mafanikio yangu ya awali. Nawapenda wote", ameandika Emanuella.

Emanuella alijizolea umaarufu sehemu nyingi Afrika, baada ya kusambaa kwa video ya vichekesho iliyopewa jina la ‘My Real Face’ na mpaka sasa amebahatika kushinda tuzo mbili za (AAMMA) nchini Australia na kutunukiwa taji la 'Princess of Comedy' na serikali ya nchi hiyo.

Kipaji cha Emanuela kiligunduliwa na mjomba wake 'Mark Angel' baada ya binti huyo  kuigiza vizuri nafasi aliyoshindwa mtoto mwingine.