Alhamisi , 19th Nov , 2015

Wasanii wa muziki wa Bongo Fleva makomando ambao pia walijipatia umaarufu kwa kucheza, wamesema kwa sasa hawawezi kucheza muziki wa msanii mwngine kwa kuwa nao wanafanya muziki.

Makomando wameyasema hayo katika kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio na kusema kwamba kwa kuwa sasa wana nyimbo zao ambazo wanaweza kucheza, hawaoni sababu ya wao kucheza nyimbo za watu wengine.

"Tuliamua kuacha kudance nyimbo za wengine kwa sababu sisi wenyewe tutacheza nyimbo zetu wenyewe, sisi wenyewe tuna kipaji cha kuimba, siwezi tena kwenda kucheza nyimbo za watu wengine, labda tuchukue dancers wetu wakacheze", alisema mmoja wa wasanii wanaounda kundi la makomando.

Pamoja na hayo wasanii hao wamesema kwa sasa mashabiki hawatawaelewa iwapo wakienda kwenye show na kucheza peke yake, kwani wengi wanawajua kuwa ni wasanii wa muziki.

Pia makomando wamesema kwa sasa wanajipanga kutoa kazi ambazo zitakuwa na ubora, ili kuweza kufikia viwango vya kimataifa.

"Watu watuamini makomando, nina imani mashabiki wetu wanataka kutuona kwenye televisheni za kimataifa, tunajipanga kwa hilo", walisema Makomando.