
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kesho, tarehe 15 Septemba 2025, itaendelae kusikilizwa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Tundu Antiphas Lissu, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Katika hatua ya kesho, Mahakama Kuu inatarajiwa kutoa uamuzi mdogo kuhusu hoja ya awali iliyowasilishwa na Lissu, akiiomba Mahakama iitupilie mbali kesi hiyo na kumuachia huru mara moja.
Aidha, Mh. Lissu aliieleza mahakama kuwa, uwasilishaji wa shauri hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ulikuwa kinyume cha sheria, hivyo uhamishaji wake kwenda Mahakama Kuu haukuwa wa kisheria. CHADEMA imesema kuwa kwa mujibu wa sheria, Mahakama haiwezi kuendesha shauri lililopatikana kwa kupokea kwa wizi au upungufu wa kisheria, na ndio msingi wa hoja yake ya awali inayolenga shauri hilo kutupwa bila kuendelea kusikilizwa.
Aidha, kimesisitiza kuwa kuheshimishwa kwa misingi ya haki, utawala wa sheria na taratibu halali za uendeshaji wa mashauri ni nguzo ya demokrasia.
Katika kuadhimisha Siku ya Demokrasia Duniani tarehe 15 Septemba 2025, CHADEMA imetoa wito kwa Watanzania wote, hususan wanachama na wapenzi wa demokrasia, kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo kwa umakinina kuongeza kuwa kinatarajia matarajio kuona Mahakama ikiheshimu na kulinda misingi ya haki na demokrasia, kwa maslahi mapana ya taifa na vizazi vijavyo.