
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limesema watu wawili ambao ni mume na mke wamefariki dunia baada ya mume,Ibrahim Shida (24), mkazi wa Kijiji cha Sirorisimba Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara, kumchoma kisu mkewe aitwaye Tatu Marwa (25), wa Sirorisimba, maeneo ya shingoni na kusababisha kifo.
Tukio hilo limetokea Septemba 12, 2025 majira ya saa 04:30 usiku ambapo Ibrahim Shida alimchoma mkewe kwa kisu maeneo ya shingo na kusababisha majeraha makubwa yaliyosababisha kifo cha mkewe baada ya kuvuja kwa damu nyingi.
Mara baada ya kutekeleza tukio hilo, mtuhumiwa alijaribu kujiua kwa kujichoma kisu shingoni na kusababisha majeraha makubwa ambapo alipelekwa hospitali kupata matibabu.
Kufuatia tukio hilo, jeshi la polisi Mkoa wa Mara linafanya uchunguzi ili kubaini chanzo chake. Aidha, jeshi la polisi limewaomba watu wenye matatizo ya kifamilia, changamoto za kisaikolojia au kiafya kuwashirikisha wanafamilia, wazee wa kimila na viongozi wa dini ili kuepusha madhara makubwa kutokea.