Jumanne , 20th Oct , 2015

Star wa muziki Jose Chameleone ameutetea msimamo wake wa kushiriki katika wimbo wa 'Tubonga Naawe' unaomsifu Rais Museveni pamoja na hafla iliyoandaliwa na kiongozi huyo kwa wasanii mwishoni mwa wiki.

Rais Yoweri Museveni akiwa na msanii Jose Chameleone

Chameleone amewataka wote wanaoona hatua hiyo sio sawa, kuacha kushikilia mtazamo hasi na kujua kuwa kila mtu ana msimamo na mawazo binafsi katika kila jambo.

Kwa upande mwingine Eddy Kenzo, msanii mwingine mkubwa Uganda, ametoa mtazamo tofauti kueleza kuwa si busara kwa wasanii waliofanya rekodi ya kumsifu Rais kumuimbia sifa tu, huku kukiwa na changamoto mbalimbali pia chini ya uongozi wake ambazo asilimia kubwa ya watu wangependa kusikia zikigusiwa pia.

Kitendo cha Rais huyo kukutana na wasanii mwishoni mwa wiki na pia kuachiwa kwa rekodi inayomsifu kumeendelea kuzua maoni tofauti kutoka kwa wasanii na Raia, kundi moja likiona ni sawa, huku la pili likiona kuwa wasanii waliofanya hivyo wameangalia maslahi yao binafsi.