Jumanne , 6th Dec , 2022

Kesi namba 12 ya mwaka 2022  inayomkabili Diana Bundala maarufu kama Zumaridi na wafuasi wake 84 ya kufanya mkusanyiko usio halali leo hii mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza imesema Zumaridi na wafuasi wake 80 hawana kesi ya kujibu huku wafuasi watatu wakikutwa na kesi ya kujibu

Akisoma maamuzi hayo Hakimu mkazi Clescensia Mushi amesema mahakama imejiridhisha pasina shaka kuwa washtakiwa walioachiwa hawakuguswa na vipengele muhimu vinavyotakiwa katika kuthibitisha makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Clescensia amewataja washitakiwa watatu waliopatikana na kesi ya kujibu kuwa ni Juma Hamisi ambae ni mshitakiwa namba 5, Meshak Joseph mshtakiwa namba 33 na Daud Manyanda mshtakiwa namba 45

Amesema washitakiwa hao ndio pekee waliotajwa na mashahidi wa Jamhuri kuwa ndio waliosababisha majeraha na maumivu makali dhidi ya askari waliokwenda nyumbani kwa mfalme Zumaridi kuwakamata Februari 23 mwaka huu.

Amesema maamuzi hayo ya kuwaachia washtakiwa 81 yametokana na upande wa Jamhuri kushindwa kujenga kesi yao yaani "Premafacie" kwani mashahidi wake  walishindwa kutambua washitakiwa kuwa walitenda makosa au la.
Baada ya maamuzi hayo hakimu Mushi akaiahirisha kesi hiyo hadi Decemba 20, mwaka huu itakapokuja kwa kwa ajili ya utetezi kwa washitakiwa watatu waliopatikana na kesi ya kujibu.

Katika hatua nyingine kesi namba 10/2022 ya kuwazuia maafisa wa serikali kutekeleza majukumu yao inayomkabili Zumaridi na wenzake nane imeendelea leo huku upande wa Utetezi ukileta mashahidi wawili kwa lengo la kutoa utetezi wao.

Mashahidi hao wametoa utetezi wao leo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Monica Ndyekobora na kuiambia mahakama kuwa waliwaona Askari polisi nyumbani kwa Zumaridi wakivunja mageti na kupiga mabomu ya machozi na kufikishwa polisi na baadae mahakamani.

Baada ya kusikiliza ushahidi huo Hakimu Ndyekora akaiahirisha kesi hiyo hadi kesho Desemba 7 mwaka huu atakapoendelea kusikiliza ushahidi kwa mashahidi wawili waliobaki.