Jumamosi , 16th Mei , 2015

Zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linaendelea mkoani Iringa huku wananchi wakitoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa kutoingilia zoezi hilo.

Baadhi ya Wananchi wakiwa katika uandikishaji wa BVR, Mkoa wa Iringa.

Mkazi mmoja wa eneo la wa Bwawani A, kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa amesema baadhi ya viongozi wa vyama wanakiuka sheria za tume ya uandikishaji kwa kuweka zaidi ya wakala mmoja kwenye kituo.

Naye Bw. Samweli Bonifasi wakala wa kituo Bwawani amesema, kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ni haki ya kila mwananchi hivyo wakala mmoja anatosha kwa ajili ya utambuzi wa wananchi wa eneo husika.

Hata hivyo, zoezi hilo kwa manispaa ya Iringa linaendelea kwa awamu ya pili katika kata za Mkimbizi, Mtwivila, Mkwawa, Mwangata na Isakalilo baada ya kumalizika kwenye kata za Kitwiru, Ruaha, Igumbilo, Nduli na mtaa mmoja wa kata ya Mkimbizi.