Naibu waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha,
Naibu waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha, ametoa agizo hilo leo mjini Dodoma alipofanya ziara kwenye machinjio hayo ili kuona utendaji kazi wake katika katika kuhakikisha kuwa inakabiliana na ongezeko la watu hasa katika kipindi hiki ambacho serikali inahamia Dodoma.
Amesema machinjio hiyo sasa ianze kufanya biashara ya nyama na kuachana na kutegemea mifugo inayoletwa na wadau na wafanyabiashara ambao mara nyingi wanaleta mifugo ambayo haina ubora.
Ameongeza kuwa nchi zote za Jumuiya ya SADC zinakabiliwa na ukame mkubwa hali inayofanya hata wanyama kufa kwa kukosa malisho hivyo kuwa na uhitaji mkubwa wa nyama.
“Nchi zote 12 za SADC zina uhaba mkubwa wa nyama kutokana na kukumbwa ukame uliosababisha kukosekana kwa malisho ya wanyama na hivyo kusababisha wanyama kufa… hivyo hiyo ni fursa kwenu ninyi kuwekeza soko lenu la nyama katika nchi hizo,” alisema Olenasha.
Kwa upande wake Kaimu meneja mkuu wa machinjio hayo, Nashoni Kalinga, amesema kuwa machinjio hayo yana uwezo wa kuchinja jumla ya mbuzi na kondoo 120 kwa siku na jumla ya ng’ombe 80 huku soko kubwa likiwa ni ndani ya mkoa wa Dodoma na nchi za Kiarabu.
Alisema sehemu kubwa ya nyama ya ng’ombe inauzwa mkoani Dodoma huku nyama ya mbuzi na ile ya kondoo zikiwa na soko kubwa kwenye nchi za kiarabu kwa kuwa nyama hizo ni za kienyeji na siyo za kisasa..
Ametaja nchi ambazo nyama ya Tanzania ina soko kubwa kuwa ni pamoja na Qatar, Oman, Dubai pamoja na Kuweit.. Ametaja nchi nyingine kuwa ni Comoro na China.