Jumatatu , 10th Aug , 2015

Zaidi ya asilimia 23 ya watanzania wametajwa kuwepo katika hatari ya kupatwa na athari za magonjwa yasiyoambukizwa ambayo huchangiwa na tabia hatarishi ikiwemo ulaji wa vyakula vyenye mafuta uzito uliokithiri na kutokuwa na tabia ya kupima mara kwa

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa taasisi inayojihusisha na upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza Dkt Lwidiko Edward ambapo amesema wamekuwa wakifanya uhamasishaji wa kupima magonjwa kama kisukari, presha, kiribatumbo kwa kuwa kuna ongezeko kubwa la watu haswa kundi la vijana wanaoathiriwa na magonjwa hayo katika umri mdogo.

Dkt. Edward ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 8 ya wagonjwa wanaopimwa hawana ufahamu kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza na kuwataka wanafamilia kujenga tabia ya kupima afya mapema haswa kwa magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakipuuzwa huku yakiwa na athari kubwa miongoni mwa nguvu kazi katika jamii.

Kwa upande wake mtaalamu na mshauri katika kampeni ya ijue afya yako bi Vanessa Chilunda ameeleza kuwa gharama za kutibu magonjwa yasiyoambukiza ni kubwa sana ndio maana wanafanya uhamasishaji haswa kwa vijana na wazazi kuweza kutambua umuhimu wa kupima afya zao mara kwa mara pamoja na kujenga nidhamu katika ulaji wa vyakula mbalimbali.

Chilunda amewataka vijana kote nchini ambao ni kundi kubwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuepuka maisha ya anasa ambayo huwaweka katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya kisukari, presha, kiribatumbo na mengineyo yanayosababishwa na ulaji mbovu wa chakula.